WATAALAM WA ELIMU KUTOKA ZANZIBAR WATEMBELEA TSC KUJIFUNZA NAMNA INAVYOFANYA KAZI

16 Feb, 2024
WATAALAM WA ELIMU KUTOKA ZANZIBAR WATEMBELEA TSC KUJIFUNZA NAMNA INAVYOFANYA KAZI

Wataalam kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Februari 12, 2024 wametembelea Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa lengo la kupata uzoefu wa namna TSC inavyotekeleza majukumu yake katika kuhudumia walimu.

Ujumbe huo ulipokelewa na Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama na kisha kufanya kikao na Menejimenti ya TSC ambapo pamoja na mambo mengine Mwl. Nkwama aliwaeleza wataalam hao kuwa Tume hiyo imeanzishwa kwa Sheria Sura 448 kwa lengo la kusimamia walimu wa Shule za Msingi na Sekondari walio kwenye Utumishi wa Umma Tanzania Bara.

“Tume yetu inasimamia masuala ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu. Tume hii inahusika na mwalimu tangu anapoingia kazini hadi anapostaafu kwa maana tunashughulika na ajira yake, tunamthibitisha kazini, tunampandisha cheo, tunambadilishia cheo pale anapojiendeleza kielimu na kutimiza vigezo, tunatoa kibali cha kustaafu lakini pia tunasimamia nidhamu na maadili yake,” alisema Katibu huyo.

 

Nkwama aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria hiyo, TSC ina ofisi katika wilaya zote 139 za Tanzania Bara ambapo ofisi hizo ndizo zinazomhudumia mwalimu moja kwa moja jambo ambalo limesaidia kurahisisha mwalimu kupata huduma.

 

Aliongeza kuwa TSC kwa kushirikiana na Mamlaka zingine imesaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa njia mbalimbali ikiwemo kuanzisha Mfumo wa Teachers’ Service Commission Management Information System (TSCMIS) ambao unamfanya mwalimu kuwasilisha changamoto zake kwa kutumia simu yake ya mkononi bila kutoka kwenye kituo chake cha kazi.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Bi. Mtumwa Iddi Hamad alimshukuru Katibu wa TSC pamoja na Menejimenti ya Tume kwa kukubali kuwapokea na kuwapa uzoefu wa namna kazi zinavyofanyika katika chombo hicho cha kuhudumia walimu.

 

Alieleza kuwa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuanzisha chambo cha kusimamia walimu tofauti na sasa ambapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ndiyo inayosimamia walimu moja kwa moja.

 

“Tumeangalia na kuona kuwa ninyi mmepiga hatua na mnafanya vizuri katika kusimamia utumishi wa walimu. Kwetu walimu ni wengi kuliko watumishi wengine wa umma, na tumegundua kuwa wizara inabeba mzigo mkubwa kitu ambacho kinasababisha usimamizi wa walimu kutofanyika kwa ufanisi. Hivyo tunakusudia kuanzisha Tume kama yenu na tumeona kuna mengi ya kujifunza kutoka kwenu kabla hatujaanzisha,” alisema Mkurugenzi huyo.

 

Wataalam wengine waliombatana na Bi. Mtumwa Iddi Hamad ni Mkaguzi Mkuu wa Elimu, Bi. Maimuna Fadhi Abass na wanasheria wawili Bw. Massoud Haji na Bw. Said Malik Juma wote kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Ujumbe huo unatarajiwa kutembelea Ofisi za TSC Wilaya ya Chamwino Februari 13, 2024 kwa lengo la kupata uzoefu wa namna ofisi za wilaya zinavyotekeleza majukumu yake.