WATAALAMU WA ELIMU NCHINI WATEMBELEA KENYA KUPATA UZOEFU WA USIMAMIZI WA WALIMU

06 Aug, 2023
WATAALAMU WA ELIMU NCHINI WATEMBELEA KENYA KUPATA UZOEFU WA USIMAMIZI WA WALIMU
Timu ya wataalamu wa elimu imefanya ziara nchini Kenya kwa lengo la kujifunza namna nchi hiyo inavyosimamia walimu ili kufanya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa walimu.
Ziara hiyo iliyofanyika Julai 25 – 29, 2023 iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Franklin Ndyetabula Rwezimula ambapo wataalamu hao walitembelea – Tume ya Utumishi wa Walimu ya Kenya na Wizara ya Utumishi wa Umma, Jinsia na Ushirikiano (Idara ya Serikali ya Utumishi wa Umma).
Wataalamu walioshiriki katika ziara hiyo iliyofadhiliwa na Mradi wa BOOST ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, John Cheyo, kutoka TSC  walikuwepo Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wakili Richard Odongo, Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu, Mectildis Kapinga na Mkuu wa Kitengo cha Mipango Ufuatiliaji na Tathmini, Evodia Pangani na kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia alikuwepo Mwalimu Mwandamizi Daudi Minja.

Taarifa ya ziara hiyo imeonesha kuwa wataalamu hao wamepata ujuzi wa masuala mbalimbali ya namna Tume ya Utumishi wa Walimu nchini Kenya inavyosimamia walimu.

“Huduma zote zinazohusu utumishi wa walimu hutolewa na chombo kimoja ambacho ni Tume ya Utumishi wa Walimu ya nchi hiyo. Hivyo, TSC nchini kenya imesaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza kwa walimu kusimamiwa na zaidi ya chombo kimoja,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Tume ya Utumishi wa Walimu nchini Kenya ndiyo Mamlaka ya Ajira na Mwajiri kwa walimu ambapo inatangaza nafasi za kazi, inaajiri, inawapangia walimu vituo vya kazi pamoja na kuwalipa mishahara.

Taarifa imeendelea kufafanua kuwa Tume ya Utumishi wa nchini Kenya ni chombo huru ambacho hakiingiliwi na mamlaka nyingine katika kusimamia Ajira, Maadili na maendeleo ya walimu, ni chombo kilichoanzishwa chini ya Katiba ya nchi hiyo.

“TSC nchini Kenya ina mifumo madhubuti ya usimamizi wa Utumishi wa Walimu jambo ambalo linaisaidia Tume hiyo kutoa huduma kwa ufanisi. Vilevile, Tume hiyo ipo chini ya Wizara ya Elimu kwa mujibu wa sera ya elimu ya nchi hiyo. Pia, Matumizi ya Mifumo ya kielektroniki katika usimamizi na utoaji wa huduma kwa walimu umeisaidia sana TSC Kenya kutoa huduma kwa ufanisi,” taarifa hiyo imeeleza.

Jambo jingine lililoelezwa na timu hiyo ni kuwa TSC Nchini Kenya inasajili na kutoa vyeti vya usaji kwa walimu wote, utaratibu huo ni wa lazima na haijalishi kama mwalimu ameajiriwa au la, ilimradi mwalimu amehitimu ualimu katika chuo cha ualimu au chuo kikuu kinachotambuliwa na Serikali ni lazima asajiliwe na chombo hicho.

TSC Kenya inasimamia Walimu katika Shule za Serikali na za kibinafsi na Mwalimu ambaye ametenda kosa la kinidhamu na kupewa adhabu ya kufukuzwa kazi hataajiriwa tena katika utumishi huo.

“Mchakato wa kuajiri Walimu na kuwachukulia hatua za kinidhamu unafanyika kwa uwazi. Walimu nchini Kenya hupandishwa vyeo kila baada ya miaka mitatu, vilevile walimu nchini humo wanapatiwa posho ya nyumba kama motisha ya utendaji kazi, hivyo Serikali haina utaratibu wa kujenga nyumba za walimu isipokuwa kwa Walimu Wakuu/Wakuu wa Shule ambao hujengewa nyumba ili kuwa karibu na mazingira ya shule”.

Kuna mengi ambayo TSC Tanzania inaweza kujifunza kutoka TSC ya Kenya katika utumishi na usimamizi wa Ualimu ili kupunguza mapengo yaliyopo katika utoaji wa huduma za walimu,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imehitimisha kwa kueleza kuwa ingawa mfumo wa kisheria uliopo wa utumishi na usimamizi wa Walimu kati ya Kenya na Tanzania unakaribia kufanana, tofauti iliyopo ni njia za utoaji wa huduma.