WAZIRI KAIRUKI AONGOZA UJUMBE WA WATAALAMU WA ELIMU KUFANYA ZIARA NCHINI SINGAPORE

06 Aug, 2023
WAZIRI KAIRUKI AONGOZA UJUMBE WA WATAALAMU WA ELIMU KUFANYA ZIARA NCHINI SINGAPORE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki ameongoza ujumbe wa wataalamu wa masuala ya elimu kufanya ziara nchini Singapore kwa ajili ya kupata uzoefu wa namna masuala ya utumishi wa walimu yanavyosimamiwa katika nchi hiyo.

Ziara hiyo iliyofadhiliwa na Mradi wa BOOST ilifanyika Julai 24 – 28, 2023 ambapo ilijikita kuangalia namna Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) nchini inavyoweza kufanya maboresho kwenye utendaji wake katika kushughulikia haki na wajibu wa mwalimu kwenye utumishi wake kwa kujifunza namna nchi nyingine zinavyotekeleza jukumu hilo.

Sababu nyingine ya kujifunza masuala ya usimamizi wa walimu katika nchi zingine ni kuhakikisha kada ya ualimu nchini inakwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea ulimwenguni ili kuwezesha wanafunzi kupata elimu inayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

“Mwalimu nchini Tanzania anatakiwa kuwa sehemu ya mageuzi ya kimataifa, na mojawapo ya marekebisho ya kimkakati yanayopendekezwa mara kwa mara, ni kuhakikisha walimu wanapangwa na kusimamiwa ipasavyo,” ilieleza sehemu ya taarifa ya ziara hiyo.

Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kuwa miongoni mwa masuala ya elimu yanavyosimamiwa nchini Singapore ni kuwa elimu ya msingi na Sekondari inatolewa katika shule za serikali pekee. Kila mwaka Idara ya Usimamizi wa Rasilimali Watu hufanya tathmini ya utendaji kazi wa kila mwalimu ambapo tathmini hiyo inatumika kama kigezo cha mwalimu kupandishwa cheo. 
“Walimu wote wameajiriwa na Wizara ya Elimu nchini Singapore baada ya kumaliza elimu ya ualimu, kupata mafunzo ya miezi sita ya kada ya ualimu na kufuzu kwa usaili. Pia, Baada ya miaka mitatu mwalimu anaweza kuhama na kufanya kazi katika taasisi nyingine na kuendelea kutambuliwa na Chuo cha Ualimu cha Singapore (Singapore Teachers’ Academy),” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. 
Jambo jingine katika usimamizi wa walimu nchini Singapore ni kuwa Mwalimu ambaye ametiwa hatiani kwa kosa lolote na kufukuzwa utumishi hawezi kuajiriwa tena katika Utumishi wa Umma. Pia, kiwango cha elimu kwa Walimu wa ngazi zote, ikiwa ni pamoja na elimu ya awali, msingi na sekondari ni kuanzia shahada ya kwanza. 

Wakiwa nchini Singapore, Waziri na ujumbe wake walitembelea Wizara ya Mambo ya Nje na Elimu, Taasisi ya Elimu, Chuo cha Walimu cha Singapore, Shule ya Msingi Noorthshore na Shule ya Sekondari Yusof Ishack.

Wataalamu walioambatana na Waziri Kairuki katika ziara hiyo ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia elimu OR – TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI, Exavier Daudi, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama na Mkurugenzi wa Idara ya Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu TSC, Mwl. Fatuma Muya.

Wajumbe wengine walioambatana na Waziri Kairuki ni Mratibu wa Mradi wa BOOST TSC, Mwl. Asha Lubuva, Afisa kutoka OR – TAMISEMI, Julius Nyalus, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Suleiman Magomba pamoja, Mwalimu Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Josephat Luoga pamoja na Afisa kutoka Ubalozi wa Tanzania New Delhi, Fanuel Mathias.