WAZIRI KAIRUKI AWASILISHA BUNGENI BAJETI YA SHILINGI TRILIONI 9 KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024

20 Apr, 2023
WAZIRI KAIRUKI AWASILISHA BUNGENI BAJETI YA SHILINGI TRILIONI 9 KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki amewasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 tarehe 14 Aprili, 2023 Bungeni Jijini Dodoma.

Waziri Kairuki aliomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 9,144,021,699,000 (Trilioni Tisa) ambazo ni matumizi ya kawaida ya Ofisi, mishahara ya watumishi, Mikoa, Halmashauri, Tume ya Utumishi wa Walimu na Miradi ya Maendeleo.

Waziri Kairuki ametoa maelezo ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kuwa katika eneo la Usimamizi na Uendeshaji wa Elimumsingi jumla ya wanafunzi wa Elimu ya Awali waliandikishwa 1,411,810, sawa na asilimia 103.52 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,363,834 ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo wanafunzi 1,500,227 wameandikishwa ikiwa ni asilimia 109.37 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,371,690 wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 2,411. 

Waziri Kairuki alisema mafanikio ya kuandikisha wanafunzi wengi kwa ongezeko la wanafunzi 88,417 sawa na asilimia 3.38 ikilinganishwa na wanafunzi walioandikishwa mwaka wa 2022 yametokana uhamasishaji wa jamii, ujenzi  wa vituo shikizi na kuendelea kutoa ElimuMsingi Bila Ada.

Kuhusu upungufu wa walimu, Waziri Kairuki amesema hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika Shule za Msingi yalikuwa 362,189 kwa kutumia uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 ambapo walimu waliopo ni 175,864 na upungufu ni 186,325 sawa na asimilia 51.44 ya mahitaji.

Aidha, alisema mahitaji ya walimu kwa Shule za Sekondari ni 174,632 ambapo waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5 lakini pia mahitaji ya walimu kwa shule za Sekondari yanatokana na masomo yanayofundishwa.

Kuhusu utekelezaji wa Afya ya Msingi, Waziri Kairuki alisema, katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 ziliidhinishwa Shilingi Bilioni 143.15 kupitia ruzuku ya Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Afya ya Msingi ambapo hadi Februari, 2023 Shilingi Bilioni 124.10 zimepokelewa sawa na asilimia 86.69 ya fedha iliyoidhinishwa.

 Waziri Kairuki alisema Shilingi Bilioni 69.95 ziliidhinishwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 15.15 ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa  kwa zahanati 300, Shilingi Bilioni 47.70 kwa Vituo vya Afya 159 na Shilingi Bilioni 7.10 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba vya afya ya kinywa, meno na macho kwa hospitali za Halmashauri 71 zilizokamilika na hadi kufikia Februari, 2023 jumla ya Shilingi Bilioni 54.55 zilikuwa zimepokelewa, sawa na asilimia 77.98.

Hadi Februari, 2023 Halmashauri zilikuwa zimekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 625.31 sawa na asilimia 62 ya makisio kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/23 ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 9.70 sawa na asilimia 1.57 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi Bilioni 615.61 yaliyokusanywa kwa kipindi kama hiki katika Mwaka wa Fedha wa 2021/22.

“Katika kuhakikisha kunakuwa na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefanyia kazi changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa mapato wa Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) kwa kusanifu na kujenga mfumo mpya wa TAUSI ambao umeanza kutumika katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23,” alisema Kairuki.