WAZIRI MCHENGERWA AITAKA TSC KUSHIRIKIANA NA HALMASHAURI ZOTE KUHAKIKISHA MICHANGO YA WALIMU INAWASILISHWA KWENYE MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KWA WAKATI

21 May, 2024
WAZIRI MCHENGERWA AITAKA TSC KUSHIRIKIANA NA HALMASHAURI ZOTE KUHAKIKISHA MICHANGO YA WALIMU INAWASILISHWA KWENYE MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KWA WAKATI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ili kutatua changamoto zinazowakabili walimu ikiwemo ucheleweshaji wa kuwasilisha michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

 

Waziri Mchengerwa alitoa agizo hilo tarehe 15 Mei, 2024 jijini Dodoma wakati wa kikao chake na Katibu Mkuu OR TAMISEMI na Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) baada ya viongozi wa TSC kuwasilisha taarifa ya zoezi la uchambuzi wa changamoto za upandishaji wa madaraja/vyeo kwa walimu.

 

Mhe. Mchengerwa alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo walimu wakati wanapofuatilia mafao yao kwenye mifuko na kukuta kuwa baadhi ya Waajiri wameshindwa kuwasilisha michango ya watumishi katika Mifuko husika.

 

Aidha, Waziri huyo aliiagiza TSC kukutana na Walimu mara kwa mara na kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kujenga uelewa kuhusiana utumishi wao.

 

Pia, aliagiza TSC kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuandaa orodha ya walimu wanaokaribia kustaafu na kuwapa elimu ya maandalizi  ya kustaafu ili kuwawezesha kuendelea kuwa na Maisha bora hata baada ya kuhitimisha utumishi wao. 

 

Aidha, Mhe. Mchengerwa aliitaka TSC kuweka mipango Madhubuti ya kujenga Ofisi za Wilaya ili kukabiliana na ukosefu wa Ofisi kwa Watumishi wa TSC katika ngazi ya wilaya na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi hao.