WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHI GARI, PIKIPIKI 62 NA KOMPYTA MPAKATO 159 KWA TSC, ATAKA MASLAHI YA WALIMU YALINDWE

01 Dec, 2023
WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHI GARI, PIKIPIKI 62 NA KOMPYTA MPAKATO 159 KWA TSC, ATAKA MASLAHI YA WALIMU YALINDWE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Mohammed Mchengerwa (Mb) amekabidhi vitendea kazi vipya ikiwemo Gari Toyota Coaster Mini Bus moja (1), Pikipiki 62 pamoja na Kompyuta mpakato 159 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa ajili ya kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa walimu.

Katika hafla ya kukabidhi vitendeakazi hivyo iliyofanyika Novemba 27, 2023 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Tambaza Jijini Dar es Salam Waziri Mchengerwa aliwataka viongozi wa Mikoa pamoja na Serikali za Mitaa kusimamia vizuri na kulinda maslahi ya Walimu na Watumishi wote Nchini wanaosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Akiongea wakati wa hafla hiyo Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa “Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini kwani zaidi ya shilingi bilioni 800 zimetumika kwaajili ya elimu bure hivyo kwa kutambua juhudi hizo inabidi tufanye kazi kwa bidii kwa kuhakikisha tunasimamia vyema miradi yote iliyopo na itakayokuja.”

“Pamoja na kusimamia miradi ni wajibu wa kila aliyepewa dhamana ya kuhudumia walimu kuhakikisha kuwa maslahi yao yanazingatiwa na kulindwa. Tukubuke kuwa ili tutoe elimu bora lazima tutengeneze mazingira bora kwa walimu kwa kuzingatia misingi aliyotuachia Baba wa Taifa ya kuhakikisha tunapambana na adui watatu yani umaskini, maradhi na ujinga. Hivyo ninawaagiza TSC kufanya Mapitio kwa walimu wote wanaostahili kupanda vyeo ili waweze kupanda kwa wakati,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.

Sambamba na hilo Mhe. Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri zao huku akisisitiza kuwa ikitokea miradi haijakamilika kwa wakati hatua za kisheria zitachukuliwa.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama ameeleza kuwa gari moja aina ya Toyota Coaster limenunuliwa kwa gharama ya shilingi 258,656,500 na pikipiki 62 aina ya Boxer kwa gharama ya shilingi 196,000,600 kupitia bajeti ya Tume huku kompyuta mpakato 159 zikigharimu shilingi 375,000,000 ambazo zimetokana na fedha za mradi wa BOOST.

Vitendea kazi utakavyovikabidhi leo ni ukamilishaji wa vile ambavyo vilianza kutolewa hapo awali. Tume ilikabidhiwa Pikipiki 81 na sasa 62 ambazo zinakamisha idadi ya pikipiki zinazotakiwa kwa kila Ofisi ya Tume ya Wilaya. Aidha, Compyuta mpakato zinazokabidhiwa leo ni vitendea kazi kwa ajili ya Makatibu Wasaidizi wote nchi nzima. Basi utakalokabidhi leo ni kwa ajili ya usafiri wa watumishi wa Tume Makao Makuu,” alisema Nkwama.