WAZIRI MCHENGERWA AWAONYA WATENDAJI WASIOWAJIBIKA, AAHIDI KUIREJESHA TAMISEMI KWA WANANCHI

06 Sep, 2023
WAZIRI MCHENGERWA AWAONYA WATENDAJI WASIOWAJIBIKA, AAHIDI KUIREJESHA TAMISEMI KWA WANANCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaonya watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao ni wabadhilifu, wala rushwa na wasiowajibika katika utendaji kazi wao hawatakuwa sehemu ya utendaji kazi wake.

Amesema atairejesha wizara hiyo kwa wananchi kwa kuhakikisha viongozi wote wanasikiliza na kutatua kero zao kwa wakati.

Mchengerwa ameyasema hayo  Septemba 4, 2023 Jijini  Dodoma mara baada ya kuwasili  katika Ofisi za TAMISEMI zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba.

“Niwaombe watumishi wenzangu kuwa sasa tunairejesha Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa wananchi, maana yake tunataka kufanya kazi hasa, ili tuweze kufanikiwa na malengo ya Mhe. Rais yaweze kutimia. Hivyo lazima tufanye kazi usiku na mchana hakuna namna. Wizara yetu tunaisogeza kwa wananchi, tutasikiliza kero za wananchi,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatoka ofisini na kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kusisitiza kuwa asilimia 45 ya wakuu wa wilaya  hawafanyi majukumu yao.

“Kuanzia sasa wakuu wa mikoa wote, wakuu wa wilaya washuke chini kusikiliza kero za wananchi, asilimia 45 ya wakuu wa wilaya hawafanyikazi kabisa, hawasikilizi kero za wananchi, kwa hiyo tunataka kila mmoja afanye kazi ili tuweze kutimiza malengo ya Watanzania, malengo ya Chama cha Mapinduzi, na malengo ya Rais wetu,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Mchengerwa amewaonya wakurugenzi wa halmashauri ambao wamekalia fedha za miradi na kusisitiza kuwa hataongeza muda wa utekelezaji wa miradi hiyo.

“Mhe. Waziri Kairuki umesema kuna miradi mingi ambayo tayari imeshaanzwa lakini kuna baadhi ya watu hawajaitimiza, uliwawekea deadline, sitaongeza hata siku moja, na nitaomba unikabidhi hayo makaratasi, kila mmoja kule aliko lazima ajue, Wakurugenzi ambao wamekalia fedha za miradi sitaongeza siku hata moja,” amefafanua  Mhe. Mchengerwa.